Jumamosi 31 Oktoba 2026 - 09:10
Nguvu ya jamii ya Kiungu huchipuka kutokana kumtumikia Mwenyezi Mungu, si katika kujitegemea na kujiona bora

Hawza/ Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Qum, akieleza kwamba Mwenyezi Mungu ameunganisha ghadhabu na ridhaa Yake na ghadhabu na ridhaa ya Bibi Fatimah (sa), ili kuwaweka Waislamu katika njia ya Mwenyezi Mungu, alisema: «Funzo letu la leo ni kwamba mihimili yote ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia na kushikamana na Wilaya ya Imam Ali (as) katika mambo yote, inapaswa kuwa na kipimo chake katika ghadhabu na ridhaa ya Bibi Fatimah (sa).»

Kwa mujibu wa taarifa ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Saidii, katika hotuba za Swala ya Ijumaa, iliyofanyika katika Muswalla Quds mjini Qum Iran, alianza kwa kutoa pole kufuatia siku za maombolezo ya Fatimiyyah, akasema: Hotuba ambayo Bibi Fatimah (sa) aliitoa katika Msikiti wa Mtume (saww) ilikuwa katika mkondo wa kufafanua na kutekeleza aya hii:

«الْیوْمَ یئِسَ الَّذِینَ کفَرُوا مِنْ دِینِکمْ فَلا تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِ»

«Leo, wale waliokufuru wamekata tamaa na dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi.»


Yaani, leo makafiri wamekata tamaa ya kuishinda dini yenu; kwa hiyo, msiwaogope.

Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Qum aliongezakwa kusema: Bibi Fatimah (sa), kupitia Msimamo wake huu wa kusimama kidete na hatua zake, alifichua waziwazi mipango na mfumo ambao wanafiki walikuwa wameubuni kwa ajili ya kuuangusha mfumo wa Kiislamu. Pia aliwakemea watu wa Madina waliovunja ahadi kwa kupuuza tukio kubwa la Ghadir Khum.

Msimamizi wa Haram Tukufu ya Bibi Fatimah Ma'asumah (sa) aliendelea kusema: Kuhusu wanafiki, kuna hatua mbili zinazopaswa kuchukuliwa:

1. Kueleza sifa zao, mipango yao na fitina zao.
2. Kuwataja na kuwabainisha watu wanaohusika nao.

Alieleza kwamba: Katika kila harakati au mapinduzi, ikiwa wanafiki hawatafichuliwa na kutengwa, husababisha madhara makubwa ambayo hayawezi kurekebishwa. Mifano ya hali hiyo tumeiona katika zama za Mtume (saww), na pia katika Mapinduzi ya Kiislamu.

Aliongeza: Katika harakati ya Uislamu, Mtume (saww) aliwafichua na kuwabainisha wanafiki kupitia aya za Qur'ani, riwaya, kueleza alama zao na baadhi ya matukio, likiwemo jaribio la kumuua Mtume (saww) wakati wa kurejea kutoka katika Vita vya Tabuk. Kwa kufanya hivyo, aliwafahamisha Waislamu wajibu wao katika suala hili.

Alisisitiza kusema: Hatua ya pili, yaani kuwabainisha watu binafsi wanaohusika na unafiki, lilikuwa ni jambo muhimu sana na nyeti lililoweza kuzua hisia na mjadala mkubwa, mazingira ya utekelezaji wake na jukumu hilo yaliwekwa juu ya mabega ya Bibi Fatimah (sa).

Hotuba na mwenendo wa Bibi Fatimah (sa), katika kipindi ambacho Imam Ali (as) alikuwa amechagua kusubiri na kunyamaza, vilikuwa katika namna ambayo viliwalazimisha wanafiki waliokuwa wamejificha nyuma ya pazia na kuvaa vinyago kufichua nyuso zao na kudhihirisha unafiki wao; ilhali wao walitaka kuudhuru Uislamu huku wakificha kabisa nia na vitendo vyao.

Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi alisema: Wanafiki katika zama za Mtume (saww) walikuwa wakitenda mambo kwa ujanja na mbinu za kutatanisha kiasi kwamba watu wengi hawakuwa na uwezo wa kuwatambua. Hali haikuruhusu hata kuwataja na kuwabainisha watu hao binafsi. Kwa sababu hiyo, watu wengi waliwaheshimu kama Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), huku watu wenye utambuzi wa kina wa mambo wakiwa katika hali ya Taqiyyah.

Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Qum aliongeza: Ibn Abil Hadid anaandika kwamba mtu mmoja alimuuliza Imam Ali (as): «Ewe Ali! Lau Mtume (saww) angekuwa na mtoto wa kiume ambaye angefikia umri wa utu uzima, je, Waarabu wangekubali mamlaka yake na kumtambua kuwa ndiye walii wao?»

Imam Ali (as) akajibu:

«لا، بل کانت تقتله»

«Hapana, bali wangemuua.»

Yaani, Waarabu hao wangemuua mtoto wa Mtume (saww).

Alieleza kwamba: Ili kukabiliana na siku kama hiyo, ambayo watu wangehitaji kuwatofautisha Waumini na wanafiki, Mtume (saww) alimweka Bibi Fatimah (sa) kuwa kipimo cha kutambua ukweli, na akasema:

«إنّ اللّه َ لَیَغضَبُ لِغَضَبِ فاطمةَ»

«Hakika Mwenyezi Mungu hukasirika kwa sababu ya ghadhabu ya Fatimah, na huridhika kwa sababu ya ridhaa yake.»

Msimamizi wa Haram Tukufu ya Bibi Fatimah Ma'asumah (sa) alisema: Hata leo, kuna baadhi ya makundi nchini Iran yanayofuatilia kupata ridhaa ya umma. Hata hivyo, yanapaswa kufahamu kwamba kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) tayari imeweka wazi kipimo cha jambo hili, kipimo hicho ni ridhaa na ghadhabu ya Bibi Fatimah (sa).

Akirejelea ukweli kwamba Mwenyezi Mungu ameunganisha ghadhabu na ridhaa Yake na ghadhabu na ridhaa ya Bibi Fatimah (sa), ili kuwaweka Waislamu katika njia ya Mwenyezi Mungu, alisema: Funzo letu la leo ni kwamba mihimili yote ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia na kushikamana na wilaya ya Imam Ali (as) katika mambo yote, inapaswa kuwa na kipimo chake katika ghadhabu na ridhaa ya Bibi Fatimah (sa).

Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Qum, akirejelea kumbukumbu ya kutekwa Jengo la Ujasusi la Marekani, alisema: Ikiwa tarehe 13 Aban 1358 ilikuwa siku ya muqawama wetu na Marekani kuhusu kufichua na kuweka hadharani ukweli wa Jengo la Ujasusi la Marekani, basi leo mapambano yetu yanahusu kuondolewa ushawishi haramu wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, mzizi wa chanzo hiki cha ufisadi utang'olewa katika eneo la Asia Magharibi.

Hotuba ya kwanza: Tafsiri ya aya za Qur'ani kuhusu taqwa na sifa za Waumini

Ayatullah Saidi, katika hotuba yake ya kwanza, akirejelea aya ya 197 ya Suratul Baqarah:

«وَ تَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَیْرَ الزَّادِ التَّقْوی»

«Na jitengezeeni zawadi, kwani hakika bora ya zawadi ni uchamngu.»

Alisema: Wafasiri wa Qur'ani wanaamini kwamba aya hii ni istiara inayorejelea safari kubwa ya maisha, yaani safari ya kuelekea kwenye mauti.

Kila tunachokikusanya kwa ajili ya safari yetu ya Akhera, ikiwa hakitaambatana na uchamungu, basi safari ya Akhera itakuwa ni safari isiyo na zawadi. Kwa sababu hiyo, kabla ya kuchukua hatua au kutenda jambo lolote kwa ajili ya Akhera, tunapaswa kwanza kufikiria kujikusanyia uchamungu.

Aliendelea na tafsiri ya aya ya 29 ya Suratul Fath, akasema: Katika aya hii, Mwenyezi Mungu, baada ya kueleza muundo wa kijamii wa Umma kupitia kauli Yake:

«أَشِدَّاءُ عَلَی الْکُفَّارِ رُحَمَاءُ بَیْنَهُمْ»

«Wenye msimamo thabiti mbele ya makafiri, na wenye kuhurumiana wao kwa wao»,

anaendelea kueleza sifa za Waumini na kusema:

«تَرَاهُمْ رُکَّعًا سُجَّدًا»

«Utawaona wakiwa katika hali ya kurukuu na kusujudu.»

Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Qum alifafanua: Mwenyezi Mungu, katika kipande cha aya kinachosema:

«أَشِدَّاءُ عَلَی الْکُفَّارِ رُحَمَاءُ بَیْنَهُمْ»

«Wenye msimamo thabiti mbele ya makafiri, na wenye kuhurumiana wao kwa wao»,

anaufafanua Umma kwa kuzingatia uhusiano wake wa nje na makafiri, pamoja na uhusiano wake wa ndani baina ya Waumini.

Kisha, katika kipande cha aya kinachosema:

«تَرَاهُمْ رُکَّعًا سُجَّدًا»

«Utawaona wakiwa katika hali ya kurukuu na kusujudu»,

anaonesha chanzo cha ndani cha uwiano huo.

Msimamo thabiti na huruma, iwapo vitatenganishwa na ibada, hugeuka na kuwa ukali na ukatili usio na roho, au hisia laini zisizo na mipaka. Kwa maneno mengine, kumtumikia Mwenyezi Mungu ndiko kunaouweka msimamo thabiti na huruma katika mkondo wake sahihi.

Aliendelea kusema: Neno «تَرَاهُمْ» (Utawaona) linaonesha kwamba sifa ya Waumini si kwamba husujudu na kurukuu mara kwa mara tu, bali wao daima wapo katika hali ya kurukuu na kusujudu, kiasi kwamba kana kwamba sura inayotawala maisha ya Waumini hao ni sura ya utumwa na unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Msimamizi wa Haram Tukufu ya Bibi Fatimah Ma'asumah (sa) aliongeza: Kurukuu na kusujudu katika aya hii si matendo mawili ya ibada yaliyojitenga tu, bali ni alama ya hali maalumu ya uwepo wa mwanadamu. Hali hiyo inaonesha kwamba jamii ya Waumini daima hujitambua kuwa iko mbele ya Mwenyezi Mungu, na kupitia uhusiano huo hupata nguvu, mwelekeo na uwiano.

Alisisitiza: Aya hii inaonesha kwamba Umma wa Qur'ani, kabla ya kusimama mbele ya adui na kuwa na msimamo thabiti dhidi ya makafiri, huwa tayari umesharukuu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na kabla haujasimama wima katika historia, huwa kwanza umeweka paji la uso wake katika sijda.

Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Qum alisema: Kurukuu ni alama ya unyenyekevu wa kutambua mbele ya utukufu wa Mwenyezi Mungu, na kusujudu ni kilele cha kujishusha na kunyenyekea mbele ya Mola Mlezi.

Kukusanyika sifa hizi mbili katika Umma kunaonesha kwamba jamii iliyobeba jukumu la utume si jamii inayojikita katika nguvu pekee, kama inavyoonekana katika ulimwengu wa leo, hususan nchi ya Marekani yenye sera za kuutawala ulimwengu. Bali, nguvu ya jamii ya Kiungu huchipuka kutokana na kumtumikia Mwenyezi Mungu, wala haitokani na kujitegemea kwa kujiona kuwa hauna haja na mwingine, wala kiburi.

Alikumbusha kuwa: Kadiri jamii hii inavyozidi kuwa na nguvu katika mwenendo wake wa kihistoria, ndivyo inavyopaswa kuwa na unyenyekevu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu, mamlaka na nguvu za kijamii haziwezi kupatikana kwa urahisi bila ya unyenyekevu huu.

Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Qum, akieleza kwamba ibada katika aya hii haimaanishi kujitenga na historia na Umma, bali ni msingi wa uwepo sahihi ndani ya historia, aliongeza: Kurukuu na kusujudu ni nguvu ya ndani inayousukuma Umma mbele, msimamo thabiti wa Umma na kuwa kwake na nguvu mbele ya makafiri hupata nguvu kutoka katika kurukuu na kusujudu. Vilevile, huruma ya Umma nayo hulishwa na ibada, wala si hisia zisizo na mizizi.

Ayatullah Saidi, akieleza kwamba aya hii haiweki pengo kati ya mambo ya kiroho na ujenzi wa jamii, alisema: Katika fikra nyingi, ibada huchukuliwa kuwa ni jambo la mtu binafsi na la faragha, huku ujenzi wa jamii ukiachwa katika maeneo ya nguvu, taasisi, siasa na utawala. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu katika aya hii haitenganishi jamii na mihrabu ya ibada.

Umma unaotakiwa ni jamii ambayo mahusiano yake ya kijamii hulishwa na ibada. Hii ina maana kwamba iwapo kurukuu na kusujudu vitaondolewa katika maisha ya jamii, hata kama kwa mwonekano wa nje nguvu na mshikamano vitaendelea kuwepo, roho ya Qur'ani itatoweka miongoni mwa watu.

Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Qum, akisisitiza kwamba kipande hiki cha aya kinaonesha kuwa utumwa kwa Mwenyezi Mungu ndio msingi wa ustaarabu wa kiimani, alisema: Kipande hiki cha aya kinaonesha kwamba ushindi wa nje haukamiliki bila ya ushindi wa ndani. Jamii ambayo hainyenyekei mbele ya Mwenyezi Mungu inaweza kuangukia katika ufisadi inapokabiliana na nguvu za kihistoria. Jamii inayosahau kusujudu, hata kama itakuwa na nguvu kwa muda mfupi, hatimaye itakumbwa na hali ya utupu na ukosefu wa maudhui ndani yake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha